Bahari Beach yafungwa, watumishi wagoma kuondoka

HOTELI ya Bahari Beach, iliyo nje kidogo ya Dar es Salaam, imefungwa huku wafanyakazi wa hoteli hiyo wakigoma kuondoka wakidai kulipwa haki zao.

Faraja Mgwabati

 

HOTELI ya Bahari Beach, iliyo nje kidogo ya Dar es Salaam, imefungwa huku wafanyakazi wa hoteli hiyo wakigoma kuondoka wakidai kulipwa haki zao. Meneja Mkuu wa Hoteli hiyo, Abbas Mang’ulo aliiambia HabariLeo kuwa hoteli hiyo yenye wafanyakazi 34, imefungwa kuanzia Jumamosi wiki iliyopita ili kupisha ukarabati mkubwa ambao utachukua miezi 10 kuanzia Februari mosi, mwaka huu.

 

Wakizungumza na HabariLeo hotelini hapo, wafanyakazi hao walisema uongozi wa hoteli hiyo uliwatangazia kuwaachisha kazi Jumamosi iliyopita kwa mdomo bila kuwapa barua. Kwa mujibu wao, walipewa kifuta jasho cha mshahara wa mwezi mmoja na nusu kila mmoja, licha ya kufanya kazi kwa mkataba tangu 2003.

 

“Hatuondoki hapa mpaka tupate haki zetu, sisi tulikuwa wafanyakazi halali wa hoteli na tupo miaka mingi iweje tulipwe fedha kidogo hivi,” alisema Mwenyekiti wa wafanyakazi hao, Jaffari Semsa. Semsa alisema walistahili kulipwa siyo chini ya Sh milioni tano kila mmoja. Alisema wanahitaji msaada wa kisheria kupata haki hiyo.

 

Hata hivyo Meneja Mkuu wa Hoteli hiyo, Mang’ulo, alisema wafanyakazi hao walikuwa katika mikataba ambayo ilikuwa haisemi kama wanastahili kulipwa haki hizo wanazodai. “Wao walikubali kusaini mikataba ambayo haikusema kama watalipwa fedha hizo wanazosema, sisi tumeamua tu kama menejimenti kuwapa asante ya mwezi mmoja na nusu, kama wanadhani wamedhulumiwa basi waende mbele,” alisema Meneja huyo.

 

Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents