Michezo

Azam FC kujipima nguvu na Mtibwa Sugar J’mosi

Katika kujiandaa na mzunguko wa raundi ya pili ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), Klabu ya Azam FC, inatarajia kukipima kikosi chake kwa kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Mtibwa Sugar utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex, siku ya Jumamosi ya Desemba 10 saa 1.00 usiku.

img_1827

Azam FC iliyoanza maandalizi ya mzunguko huo wa pili Jumatatu iliyopita, itautumia mchezo huo kuwapima wachezaji wake kabla ya kuanza mikikimikiki ya ligi, ambapo inatarajia kufungua pazia kwa kucheza na African Lyon Desemba 18 mwaka huu kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Baadhi ya wachezaji wapya itakaowatumia katika mchezo huo ni washambuliaji Yahaya Mohammed (Aduana Stars) na Samuel Afful (Sekondi Hasaacas), ambao wametua nchini hivi karibuni wakitokea nchini kwao Ghana sambamba na beki wa kati, Yakubu Mohammed (Aduana Stars) aliyekuja kufanya majaribio ya kujiunga na Azam FC.

Mabingwa hao wanawafanyia majaribio wachezaji wengine wawili kutoka Cameroon, beki wa kati Batetakang Flavius (Canon Yaoundé) na kiungo mkabaji Stephane Kingue (Coton Sport FC de Garoua), ambao nao wanatarajia kuwemo kwenye mtanange huo.

Hadi inamaliza raundi ya kwanza ya ligi, Azam FC, imeshajikusanyia jumla ya pointi 25 katika nafasi ya tatu kwenye msimamo ikiwa nyuma pointi 10 dhidi ya Simba (35).

Mbali na kujiandaa na mzunguko wa pili wa ligi, Azam FC pia inayatumia mazoezi hayo kujiandaa ipasavyo na michuano mingine ya Kombe la Mapinduzi, Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) na Kombe la Shiikisho Afrika (CC), ili iweze kufanya vizuri.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents