Habari

Askofu Gwajima asimulia A to Z ya ilivyokuwa polisi

Kanisa la Ufufuo na Uzima linaloongozwa na Askofu Josephat Gwajima limetangaza vita dhidi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwa kumtaja katika orodha ya wanaojihusisha na dawa za kulevya, jambo ambalo alisema limethibitika si la kweli.

Gwajima alisema hayo Jumapili hii katika ibada ya Jumapili iliyofanyika kanisani kwake, Ubungo Dar es Salaam.

“Unajua safari hii Ufufuo na Uzima hatujachokoza mtu, hatujachokoza mtu ila tumechokozwa. Nataka niwaambie naomba mnisikilize kwa makini sana, najua kila mtu anapenda kusikia nini kimetokea na mimi sitaanza na mahubiri kwanza,” alisema huku akishangiliwa na waumini wake. Hebu msishangilie kwanza, halafu mnisikilize, nitaanza kuwafafanulia nini kimetokea.”

Aliwaambia waumini wake kuwa wanafurahi kwa kuona baba yao amerudi, lakini furaha haijakamilika kama wengine walioonewa wako huko. “Leo wewe unafurahi kwa kuniona mimi nipo hapa lakini kuna wengine nimewaacha kule ambao hawana sauti kama mimi, sasa leo mimi nitakuwa sauti yao,” alisema na waumini wake wakamshangilia.

“Niliamua kufanya ziara hiyo kwa helikopta ili kurahisisha kazi, kwamba naweza kuondoka Jumatano na kurudi nikiwa sijachoka. Niliondoka siku hiyo hadi Mpwapwa lakini siku hiyo hakufanya mkutano kwani lengo lilikuwa kuwatembelea wachungaji. Alisema baada ya dakika 40 alikwenda Chamwino na akiwa hewani, alisikia tangazo kuwa Makonda amemtaja. Nilichukua uamuzi wa kufuta safari maana kama umetajwa unaweza kukutana na mtu ambaye si mwelewa akakutendea vibaya kwa sababu amesikia mtu fulani amekutaja,” alisema.

“Usiku mzima ule nilikuwa natafakari kwa nini mkuu wa mkoa ameamua kufanya hivi kwa mtu wa aina yangu, maana watu wote aliowataja ni wanasiasa na wafanyabiashara ila mchungaji ni mimi, “alisema huku akiwa na mshangao.

“Niliwafafanulia viongozi hao wa kanisa kisha nilikwenda polisi, nilimkuta Yusuf Maji, sijawahi kukutana naye tulisalimiana na kutambulishana,” alisimulia.

Alisema baada ya hapa walionana na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro na kumweleza mambo machache kuhusu Makonda na sakata la shisha alivyotuhumu viongozi kuwa wameiruhusu. Baada ya maelezo hayo alimtaka Sirro amweleze alichomuitia. Kamanda huyo alimtaka waende kwa mkemia mkuu kupima mkojo na damu ili kubaini kama anatumia dawa za kulevya. “Mimi na mheshimiwa Manji tuliambiwa twende kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kupimwa, nilikubali na kuwaambia twende na hata mkikuta pombe semeni mmekuta dawa za kulevya,” alisema.

Alisema walichukua sampuli na kupimwa kwa uwazi wala hawakuficha na baada ya vipimo majibu yakaonyesha hakuna chochote.”Baada ya majibu hayo wakaniambia wakachunguze nyumbani kwangu, niliwaambia twende, tuliondoka usiku huo hadi nyumbani kwangu. Kabla sijaendelea kueleza, naomba msiwalaumu Jeshi la Polisi, wala Ofisi ya Rais ni kiumbe mmoja tu ameingilia kati hapa anayesababisha maneno yote haya, hii siyo issue (suala) ya Serikali ni issue ya kiumbe,” alisema.

Alisema waliongozana na askari hadi nyumbani na kuwaambia mkikuta hata sigara semeni mmekuta dawa za kulevya. “Waliingia kwenye nyumba yangu ya ghorofa tatu na kuchunguza kila kitu, karatasi kwa karatasi droo kwa droo.”

Waliitwa na majirani ili kuweka ushahidi na kuchunguza mpaka saa nane usiku, lakini mwisho hawakukuta kitu… Walikuta hati za ndege na vitu vya kawaida tu.”

Alisema baada ya kujiridhisha wakarudi polisi kuendelea na mahojiano ambako walimuuliza kuhusu utajiri alianao, “Niliwaambia nendeni kwenye akaunti zangu na nikawaambia mimi ni daktari wa filosofia, mimi ni mwandishi wa vitabu na hadi sasa nina vitabu 37, silali nafanya kazi halafu mtu mmoja kakaa kwenye kiti chake anakurupuka na kusema.”

Alisema walipekua akaunti yake na kugundua hakuna kitu, “Sasa dawa hakuna, vipimo vimeonyesha hakuna utafanyaje sasa jina la Gwajima nililolijenga kwa miaka 29 utalifanyaje, utalioshaje?” alihoji.

Baada ya kueleza hayo alisema hataipeleka Serikali mahakamani, bali atamshtaki Makonda kwa Rais na kwamba kama Makonda ataendelea kuwa mkuu wa mkoa hatakubali. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam bado anaendelea na mapambano dhidi ya dawa hizo katika mkoa huo.

By: Emmy Mwaipopo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents