Annan njia panda Kenya

Wakati aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (U.N.), Bw. Kofi Annan kwa mara ya pili jana alikutana na kiongozi wa Orange Democratic Movement (ODM), Bw. Raila Odinga katika juhudi za kutafuta amani nchini Kenya, imearifiwa kuwa, watu 10 wameuawa siku hiyo hiyo katika mapigano makali ya kikabila kwenye mji wa Naivasha uliopo kwenye eneo la Bonde la Ufa, limeandika Shirika la Habari la Uingereza, Reuters ja

Na NAIROBI, Kenya

 
Wakati aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (U.N.), Bw. Kofi Annan kwa mara ya pili jana alikutana na kiongozi wa Orange Democratic Movement (ODM), Bw. Raila Odinga katika juhudi za kutafuta amani nchini Kenya, imearifiwa kuwa, watu 10 wameuawa siku hiyo hiyo katika mapigano makali ya kikabila kwenye mji wa Naivasha uliopo kwenye eneo la Bonde la Ufa, limeandika Shirika la Habari la Uingereza, Reuters jana.

 

Hadi sasa, inakadiriwa kwamba, watu 750 wameuawa katika maeneo tofauti nchini Kenya tangu kuzuka kwa ghasia zilizofuatia uchaguzi mkuu uliofanyika nchini humo, Desemba 27, mwaka jana na baadaye Rais Mwai Kibaki kutangazwa na Tume ya Uchaguzi Kenya (ECK) Desemba 30 mwaka kushinda.

 

Mwandishi wa habari wa Reuters mjini Nairobi, alithibitisha kuhesabu maiti 10 jana, miongoni mwao sita wakiwa na majeraha ya moto na nyingine nne zilizokuwa na majeraha ya vipigo kutoka kwa watu wa kabila la Wakikuyu wanaoaminika kumuunga mkono Rais Mwai Kibaki dhidi ya makabila mengine ya Waluo na Wakalenjin.

 

Malori mawili yaliyokuwa yamejaa askari, yalipelekwa katika eneo la ghasia ili kutuliza vurugu hizo, huku moshi mzito ukifuka kufuatia majengo na magari ambayo yalikuwa yamechomwa moto.

 

Vizuizi vilivyowekwa na watu hao katika barabara kuu iendayo Magharibi mwa Kenya, iliwalazimisha polisi kutafuta njia nyingine ili kuweza kulifikia eneo hilo lililokuwa na ghasia.

 

Muendelezo wa machafuko ya jana mjini Naivasha sasa yanauweka njiapanda upatanishi uliokuwa ukiendelezwa jana na Bw. Annan kutaka serikali ya Rais Kibaki na ODM kuteua majina ya maafisa wawili kila upande kwa ajili ya majadiliano zaidi ya kutafuta amani nchini humo.

 

Awali jana, Bw. Annan alifanya mazungumzo kwa mara ya pili na Bw. Odinga yakilenga namna ya kutafuta suluhu ambayo inaweza kusimamisha ghasia zinazoendelea na maafa nchini humo.

 

Hali kadhakika, kiongozi huyo mstaafu wa UN, juzi alitembelea maeneo yaliyoathiriwa na mapigano ya kikabila katika Bonde la Ufa na kusema kuwa kulikuwepo na ukiukwaji mkubwa wa haki.

 

“Tusijidanganye hata kidogo kwa kusema kwamba hili ni tatizo la uchaguzi pekee kwa sababu shida hii ni pana zaidi,“ alisema Bw. Annan.

 

“Inatulazimu kutafuta ufumbuzi wa masuala ya msingi kwanza kufuatia haya tunayoyaona leo hii, kwani vinginevyo, ndani ya miaka mitatu au mitano kuanzia sasa hali mbaya itajirudia upya,“ alisema.

 

Kuzuka kwa ghasia na mauaji mjini Naivasha jana na mengine kwenye mji wenye vivutio kwa watalii wa Nakuru usiku wa Alhamisi iliyopita, kumeendelea kuzua wasiwasi mkubwa nchini Kenya.

 

Baadhi ya wananchi wa Kenya wanadhani kwamba viongozi wote wa pande zinazopingana nchini humo, hawaonyeshi juhudi kubwa za kusimamisha tofauti hizo za kikabila zinazohusisha uhasama wa umiliki wa ardhi, uroho wa madaraka na biashara.

 

“Uchaguzi umeweza kuibua hadharani chuki ambazo zilikuwa zimejificha kwa miaka mingi,“ ameandika Gitau Warigi katika safu yake ndani ya gazeti la Sunday Nation jana.

 

Utafiti uliofanywa na gazeti hilo kwa watu 2,000 jana, umeonyesha kwamba asilimia 51.6 wanaamini kwamba, Bw. Annan anaweza kufanikisha upatanishi wa mgogoro wa Kenya.

 

Alhamisi iliyopita, Bw. Annan alifanikiwa kuwakutanisha ana kwa ana mahasimu wa uchaguzi huo katika kiti cha Urais, Rais Kibaki na Odinga tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu uliotawaliwa na utata katika kura za urais mwaka jana.

 

Hata hivyo, muda mfupi baada ya viongozi hao kushikana mikono mjini Nairobi huku wakitabasamu, ghasia na mauaji yaliibuka mjini Nakuru huku kila upande ukituhumu upande mwingine.

 

Inakadiriwa kwamba hadi sasa, tangu kufanyika kwa mazungumzo hayo ya amani Alhamisi iliyopita, mapigano ya kikabila yanayotumia mapanga, mikuki, pinde na mishale mjini Nakuru, yamesababisha vifo vya watu 27.

 

Vyombo mbalimbali vya habari nchini Kenya vinasema kwamba idadi ya watu waliouawa mjini Nakuru tangu Alhamisi inafikia 50.

 

Uhasama huo unahusisha makabila ya Wakikuyu wanaopingana na Wakalenjin, Waluo na Waluhya wanaosadikiwa kumuunga mkono Odinga ambapo kila upande katika eneo la Bonde la Ufa umedhamiria kulipiza visasi.

 

Miongoni mwa waathirika wa machafuko hayo ni Bw. Cosmas Monyao ambaye anasema kuwa biashara yake ya kuuza kofia kwa watalii imeshuka mno.

 

“Mimi sijali mtu anatoka kabila gani bali kimsingi machafuko haya yameniharibia mno biashara yangu,“ amesema Monyao.

 

“Kama Rais Kibaki na Odinga wana hamu ya kupigana kwa nini wasiingie jukwaani na kupigana wenyewe kwa wenyewe,“ alihoji mjasiriamali huyo.

 

Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents