Michezo

Angurumapo Simba Mcheza ni Yanga

 

YANGA jana iliendelea kuinyanyasa Simba msimu huu baada ya kuichapa bao 1-0 katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.

Simba inafungwa kwa mara ya pili mfululizo baada ya kuchapwa mabao 3-1 kwa mikwaju ya penalti katika mechi ya Ngao ya Hisani iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Jerryson Tegete ndiye alipeleka msiba kwa mabingwa hao watetezi, Simba, baada ya kufunga bao hilo katika dakika ya 70 baada ya kuwatoka mabeki wa Simba na kumchambua kipa Juma Kaseja wa Simba kabla ya kuujaza mpira wavuni.

Katika kipindi cha kwanza cha mechi ya jana, Simba walianza mpira kwa kasi na kufanya shambulizi zito katika dakika ya tatu ambapo Emmanuel Okwi akiwa na kipa Yew Berko alishindwa kufunga baada ya kipa huyo wa Ghana kuucheza mpira na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Baada ya kosakosa hizo za Simba, Yanga walitulia na kuanza kupanga mashambulizi langoni mwa Simba, hata hivyo, washambuliaji wake hawakuwa makini kuweka mpira kimiani.

Simba walianza kipindi cha pili kwa kasi na kufanya shambulizi lililozaa kona lakini haikuzaa matunda.

Na katika kipindi hicho ndipo mabadiliko yaliyofanywa na kocha wa Yanga, Kostadin Papic kwa kuwatoa Abdi Kassim na Athumani Iddi ‘Chuji’ na kuwaingiza Geofrey Bonny na Yahaya Tumbo yalipozaa matunda kwani yalionekana kuamsha ari na Yanga kufanya mashambulizi mfululizo langoni mwa Simba.

Akizungumzia mechi hiyo, kocha wa Simba Patrick Phiri alisema amekubali matokeo na kwamba wachezaji wake wangeweza kushinda kama wangetumia vizuri nafasi walizopata katika kipindi cha kwanza, kwa vile ndio walicheza vizuri zaidi.

“Lakini katika kipindi cha pili wachezaji wangu walionekana kushindwa kucheza hasa katika dakika za mwisho na hapo ndipo Yanga walipotumia makosa hayo kupata bao lililowapa ushindi,” alisema na kuongeza kuwa hana wasiwasi na mwamuzi Ramadhani Kidiwa kwani alichezesha vizuri.

Naye kocha wa Yanga, Papic alisema ameridhishwa na matokeo na kukiri kwamba Simba waliwazidi katika kipindi cha kwanza lakini aliwapa maelekezo wachezaji wake walipokuwa mapumziko na kubadilika kipindi cha pili kilichozaa bao la ushindi. Kwa ushindi huo, Yanga inaongoza ligi kwa pointi 19 ikifuatiwa na Simba yenye pointi 16.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents