Habari

Aliyemtishia bastola mheshimiwa Nape si polisi – Mwigulu

Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba amesema mtu aliyemtishia kwa bastola aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye si askari wa Jeshi la Polisi, lakini ameshapatikana na atashughulikiwa kwa mujibu wa utaratibu wa ulinzi na usalama.


Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba

Mwigulu alisema hayo baada ya kufungua mkutano wa kazi wa mwaka wa maofisa waandamizi wa polisi, makamanda wa mikoa na wakuu wa vikosi wa Jeshi la Polisi ambao unafanyika mjini hapa. “Ameshapatikana (aliyemtishia Nape) na atashughulikiwa kwa mujibu wa taratibu za ulinzi na usalama ambazo zimekuwa zikifanyika ndani, lakini hazitangazwi,”alisema.

Hata hivyo, Mwigulu alikataa kuelezea kwa undani kuhusu mtu huyo kwa kubainisha anatoka taasisi gani wala jina la mtuhumiwa kwa madai kuwa ni kwa sababu ya usalama wake. Mtu huyo alifanya kitendo hicho wakati Nape, ambaye alikuwa Waziri wa Habari, alipokuwa anaelekea Hoteli ya Protea alikopanga kuzungumza na waandishi wa habari baada ya mbunge huyo wa Mtama kuachwa katika mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri.

Mtu huyo alikuwa pamoja na wenzake wawili ambao kwa pamoja walikuwa wakimlazimisha arudi kwenye gari lake na kuondoka, lakini Nape alibisha na ndipo mtu huyo aliporudi nyuma, kuchomoa bastola kutoka kiunoni na kisha kumtishia kabla ya kutulizwa na mwenzake.

Watu hao walitoweka eneo hilo muda mfupi baadaye. Siku moja baada ya tukio hilo Mwigulu alimwagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi, Ernest Mangu kumtafuta mtu huyo.

Na Emmy Mwaipopo

Chanzo: Mwananchi

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents