Aliyempiga Mwinyi ajutia kitendo chake
KIJANA Ibrahimu Said Sultan “Ustadhi” (26), ambaye juzi katika sherehe za Maulid alimpiga kofi Rais mstaafu wa awamu ya pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi, ameliambia Jeshi la Polisi nchini kuwa anajutia kitendo hicho.
Alisema kofi alilompiga kiongozi huyo halikulenga kumdhuru, bali alifanya hivyo kama njia ya kufikisha ujumbe kwa watu wengi dhidi ya matamshi ya viongozi wa dini.
Ibrahimu alisema ujumbe aliotaka uwafikie watu wengi ni ule wa kupingana na hotuba za viongozi wa dini ya Kiislamu, zinazosisitiza Wakristo na Waislamu kushirikiana katika kuadhimisha sherehe za kidini, ikiwamo Krismasi, Maulid, Iddi na Pasaka pamoja na matumizi ya kondomu ambayo kwa Waislamu ni sawa na kuhalalisha zinaa.
{seyretpic id=857 align=right}Kamanda wa Polisi Kanda Maalum, Dar es Salaam, Suleiman Kova, alieleza kauli ya kijana huyo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari na kueleza kuwa, Jeshi hilo linasubiri majibu kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili ambayo inampima kama ana akili timamu ili aweze kupandishwa kizimbani.
Akifafanua zaidi juu ya nia ya Ibrahimu kufanya kitendo hicho, Kova alisema alipofanya mahojiano naye baada ya kupelekwa kituo cha polisi, kijana huyo alidai anampenda Mzee Ruksa, hivyo hakuwa na nia mbaya, bali aliona ujumbe wake ungeweza kuwafikia wengi kwa kufanya kitendo hicho alichokiita kituko.
“Mtuhumiwa alipohojiwa kuhusu tukio hilo, alieleza kwamba hakuwa na lengo lolote la kumdhuru Rais Mstaafu, bali alikuwa na lengo la kufanya kituko chochote kile ili ujumbe wake uwafikie watu wengi.
“Alidai hakubaliani na hotuba za viongozi wa Kiislamu zinazowasisitiza Waislamu na Wakristo kushirikiana katika kuadhimisha sherehe za kidini kama vile kusherehekea kwa pamoja sikukuu za Maulid, Iddi, Pasaka na Krismasi,” alisema Kova.
Alisema mtuhumiwa huyo alikuwa na maoni tofauti dhidi ya wito huo, kwani alitaka dini hizo mbili kila moja iadhimishe sikukuu zake bila ya kuwapo kwa ushirikiano kama ilivyokuwa ikisisitizwa.
Kwa mujibu wa Kamanda Kova, kijana huyo, ambaye ni mwalimu wa masomo ya ziada katika kituo cha Ngome Kongwe, Mabibo, jijini Dar es Salaam, alijutia kitendo alichomfanyia Mzee Mwinyi ila hakuwa na njia nyingine ya kufikisha ujumbe wake.
Kova alieleza kuwa, tukio hilo halikutarajiwa kutokea eneo hilo ikizingatiwa mazingira yake yalikuwa ya kidini.
Wakati huo huo, Taasisi ya Kiislamu ya Taibah, imetoa taarifa kwa vyombo vya habari na kulaani kushambuliwa kwa Rais Mwinyi na kutoa pole kwake, kwa serikali na uongozi wake.
Wananchi hao walisema kitendo hicho kimeipaka matope Idara Usalama wa Taifa iliyo nyeti hapa nchini.
“Huo ni uzembe wa Usalama wa Taifa, hawazingatii uwajibikaji, haiingii akilini kwa kijana yule kuachiwa kupenya hadi meza kuu na kumfikia Rais Mstaafu. Endapo kijana yule angekuwa na bastola au silaha nyingine yoyote, leo hii tungezungumza mengine,” alisema Rashid Tunguli.
Katika taarifa ya Taasisi ya Taibah, iliyosainiwa na Mwenyekiti wake, Sheikh Ali Mubarak, kwa niaba ya taasisi hiyo, alisema Rais Mwinyi ni mzee mwenye busara anayetegemewa, hivyo kumfanyia fujo ni kitendo cha kinyama ambacho si utamaduni wa Tanzania, kinapaswa kulaaniwa na kudhibitiwa ili kisitokee tena.
Taibah iliishauri serikali kuchukua hatua kali dhidi ya kitendo hicho na kupata undani wa tukio hilo. Walimwomba Mungu kumlinda rais huyo mstaafu pamoja na viongozi wote wa serikali dhidi ya watu wasiowatakia mema.