Burudani

Ali Kiba vs Diamond: Badala ya kulumbana, fanyeni kolabo au tour mpige hela!

Vita ya chini kwa chini kati ya Ali Kiba na Diamond Platnumz iliyopo kwa miaka mingi, imeibuka tena na huenda safari hii ikawa kubwa zaidi kama hapatatokea suluhisho. Ali Kiba na Diamond hawasemeshani kwa muda mrefu na hata ule mradi wa Kigoma Allstars uliowakutanisha kwaajili ya kurekodi nyimbo, haukufanikiwa kuwasuluhisha.

page

Mengi yamekuwa yakiongelewa kuwa chanzo cha kutoelewana kwao yakiwemo masuala ya kishirikina ambapo Ali Kiba amewahi kudaiwa kumtuhumu hitmaker wa ‘Mdogo Mdogo’ kuwa anatembelea nyota yake. Wasanii wengine pia akiwemo Q-Chief, wamewahi kudai hivyo.

Juhudi za kuwapatanisha hazijawahi kufanikiwa na kuna wakati Joseph Kusaga aliahidi kuwaweka mezani.

‘Tension’ kati ya wawili hao ilianza tena wiki iliyopita kupitia promo ya kipindi cha ‘The Sporah Show’, ambapo Sporah alimuuliza Alikiba kama Diamond ndiye amechukua nafasi yake kwenye muziki kwa kipindi alichokaa kimya.

Alikiba alijibu kuwa Diamond hajachukua nafasi yake, na kusindikiza jibu lake na mfano wa (nafasi yake) ni sawa na kiti kilichopata vumbi (kwa kutokaliwa siku nyingi) hivyo muda wowote akiamua kurudi anaweza kuamua kukifuta na kukikalia tena. Pia aliongeza kuwa Diamond amekaa kwenye kiti tofauti na yeye, lakini yuko ‘back seat’.

Pia kupitia 255 ya kipindi cha XXL, July 17, Alikiba aliulizwa swali kuhusu yukoje sasa hivi na Diamond ana alijibu:

“Mimi niko okay sana sema sifikirii kuongea naye tu basi lakini niko very okay yaani. Yaani sijawahi kufikiria si unajua kuwa na mtu okay ni kuzungumza na kuwa karibu unajua hivyo vitu, yaani sijawahi kufikiria hata hivyo. Mi niko okay na sina chuki na sana sana nampongeza lakini sina chuki, simaind yaani niko veeery okay”.
Kauli hiyo ya Ali Kiba ikazua maswali mengi ya kwamba kama hana tatizo naye kwanini hafikirii kuongea naye?

Jumapili ya July 20, Diamond Platnumz aliandika kupitia Instagram kile kilichotafsiriwa na wengi kuwa ni jibu kwa Ali Kiba. “Tatizo lako wewe unawaza kushindana na mimi ili nishuke… Wakati mwenzako nawaza kushindana na watu wa mataifa Mengine ili nilete Sifa na Heshima Nchini kwetu,” aliandika staa huyo.

Historia inaonesha kuwa pamoja na Ali Kiba kuwahi kushiriki kwenye miradi mingi ya kimataifa ukiwemo ule wa ‘One 8’ ambao ulimkutanisha na wasanii wa kimataifa akiwemo R-Kelly, Diamond Platnumz amefanikiwa kwenda mbali zaidi. Naturally, mafanikio ya Diamond ni ‘mwiba’ unaomsumbua Ali Kiba. Bahati mbaya na ukweli ulio wazi kuwa itachukua nguvu, pesa na jitihada nyingi kwa Ali Kiba kuweza kufikia kiwango alichofika Diamond kwa sasa.

Hii ni kwasababu Diamond hana tena mtu wa kushindana naye Tanzania kama si Afrika Mashariki (ukimtoa Jose Chameleone). Alipo Diamond leo hii ni sehemu ambapo anashindana na wasanii wakubwa barani Afrika wakiwemo Davido na wengine. Na ndio maana kutokana na ukubwa wake sasa, wasanii wakubwa wamekuwa wakiomba kufanya naye collabo na sio vice versa.

Na pia waswahili husema ‘kutangulia sio kufika’. Hivyo ile mitazamo ya ‘yule si kaja juzi tu’ imekuwa ikiwaponza wasanii wengi na kusahau kuwa kuanza haimaanishi utakaa juu milele.

Hakuna anayebisha kuwa Ali Kiba ni muimbaji mwenye uwezo mkubwa, lakini tangu ‘Single Boy’ aliyomshirikisha Lady Jaydee, hajawahi kutoa hit nyingine tena. Single Boy iliwahi kushika nafasi ya 3 kwenye chart ya kituo cha radio kinachosikilizwa zaidi kwenye mji mkuu wa kibiashara nchini Nigeria, Lagos, The Beat 99.9 FM.

Pamoja na hivi karibuni kushirikishwa kwenye nyimbo nyingi, katika kipindi cha miaka miwili, hakuna wimbo wa kutisha uliotoka kwake.

Nani mkali kati ya Diamond na Ali Kiba?

Kwa mujibu wa mtangazaji mkongwe wa redio nchini, Masoud Masoud, kupendwa na kuwa na kipaji ni vitu viwili tofauti, na anaamini Ali K ni mkali kuliko Chibu.

“Mimi wa kwanza nitakayempendekeza aaah nani huyu, nampenda sana katika wasanii wote wa bongo fleva, Alikiba, Alikiba nampenda sana. Alikiba kama umemsikiliza, rhyme zake zile katikati ya zile bars anavyoimba ni mwanamuziki kama angekuwa nje ya nchi asingekamatika. Angepata producer mzuri wa kumfahamisha nini cha kuimba beat gani atumie, Alikiba yuko juu sana,” Masoud alikiambia kipindi cha Mkasi.

Kuhusu Diamond, Masoud alisema:

“Nyota imeng’aa kwa Diamond Platnumz lakini Diamond Platnumz siwezi kumlinganisha hata kidogo na Alikiba, kwenye kuuza huwezi kumlaumu anaweza kuwa Diamond akauza sana au akampandisha na si Tanzania tu, hata Hollywood wanafanya hivyo hata CBS wanafanya hivyo, hata US music industry wanafanya hivyo. Sasa mpaka wakiwepo watu wataalam wanaoweza kusema huyu anaimba sawa huyu haimbi sawa lakini kwenye mauzo hakuna mtu anajali hilo.”

Katika muziki, malumbano kati ya wasanii wawili wakubwa, yanaweza kuwa na faida kibiashara kama yakitumiwa vyema. Kwa kinachoendelea kati ya Diamond na Ali Kiba, wote wanaweza kunufaika ‘locally’ kama wakiamua kushindana kwa ‘vitendo’ na sio ‘maneno’. Bahati nzuri kwa Diamond ni kwamba siku zote amekuwa mtu wa vitendo na huku ukimya wa Ali Kiba ukionekana kuwa tatizo.

“Inategemea na plans, unajua kuna kimya ambacho kinajenga na kimya ambacho kinabomoa,” anasema DJ Majay (EFM, E-Masters, Maisha Club).

“Kwahiyo yeye kama amekaa kimya kwa malengo, siwezi kusema kama amepotea, lakini kama amekaa kimya ambacho hakina malengo naweza kusema amepotea. Lakini wengi wanafanya vitu kwa mahesabu kwahiyo mahesabu yake ndio yata determine kujua kama anapotea au anajijenga. Kwa mfano mimi kimya chake hicho akikaa halafu akachomoza na kitu kikali, ofcourse kinafutika ndani ya siku moja tu. Kwa mtazamo wangu mimi naona Ali Kiba bado anayo nafasi, inategemea na hesabu zake anazozifanya. Kwasababu muziki ni biashara, lazima ajue anamlenga nani na kwa muda gani. Kwahiyo akijipanga bado ana nafasi kubwa tu sababu bado ni msanii mkubwa.”

“Mimi nimepata nafasi ya kukutana na Watanzania mbalimbali kwa mfano kama South Africa nilikuwa naenda mpaka kwenye club ambazo watanzania wapo,” anasema mtangazaji anayependwa katika tuzo za watu 2014, Millard Ayo wa Clouds FM.

“Dubai nilipata nafasi ya kuwauliza watu muziki gani wa Tanzania wanaupenda kiukweli Ali Kiba alitajwa zaidi. Kwahiyo inaonesha ni jinsi gani bado ana nafasi. Kuna sehemu kama Dubai, nilienda sehemu nikawa nauliza watu, bado watu wengine hawawajui akina Diamond. Kwa mfano kuna wakenya niliwauliza ‘msanii gani wa Bongo Flava unampenda’ bado wao wapo na wale wasanii kama Afande Sele, Ali Kiba. Kwahiyo bado ana nafasi, Mimi simlaumu kwa ukimya wake kwasababu wakati mwingine mtu anaweza akawa ameamua kuwa kimya kwasababu ya kujipanga kwa mambo yake na anaweza akaja na kishindo kikubwa au akaja na moto mkubwa kwenye kazi yake,” anaongeza.

“So ukimya wake unaweza ukawa sahihi wakati mwingine au unaweza usiwe sahihi. Lakini kama amekaa kimya kwasababu ya kujiandaa na kazi yake hapo inawezekana ikawa sahihi kabisa kwasababu sasa hivi kwenye bongo flava kuna competition sio kidogo. Watu sasa hivi hawako kwa msanii mmoja tu ukija na kazi nzuri watu wanahamia kwako. Wasanii ni wengi na wengi wameamua kuifanya kama ajira baada ya kuona mifano hai kwa wasanii wengine wanaofanikiwa wanajenga nyumba zao, wanaonesha mali zao, wanapata madeal makubwa kwahiyo watu wameamua kuwa serious.”

Mwisho wake ni upi? Muda utatupa jibu.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents