Bongo5 Exclusives

Akothee: Msanii wa Kenya aliyepitia udereva ma3/taxi hadi kumiliki kampuni ya tour na nyumba za kupanga (Video)

Kwa msichana mwingine, kuachwa na mume aliyekuwa akimtegemea kwa kila kitu na kuachiwa watoto wadogo wanaohitaji kula na kwenda shule, kingekuwa chanzo cha kuamua kwenda kufanya kazi hatarishi ikiwemo kujiuza mwili wake. Hata hivyo, kwa Esther Akoth Kokeyo anayejulikana kwa jina la muziki kama Akothee, hali ilikuwa tofauti.

“Nilipopata talaka niliona maisha yamenikatikia,” Akothee aliambia Bongo5 kwenye mahojiano maalum jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita ambako alikuja kujitangaza.

“Maana yake nilikuwa namtegemea baba yake watoto wangu kwahiyo alivyonitupa nje maisha hayakuwa rahisi tena vile nilivyokuwa nayaona.” Wakati anapewa talaka, Akothee alikuwa ndio amemaliza shule kwakuwa aliolewa akiwa na umri mdogo, hivyo aliamua kuwa dereva wa matatu huku akijisomesha mwenyewe kwenye chuo cha udereva.

Anadai aliamua kufanya kazi hiyo kwakuwa inaonekana kuwa ni kazi ya wanaume zaidi na hivyo ikawa rahisi kupata kazi. Aliamua kuhamia Mombasa ambako alipata kazi ya hoteli huku akitengeneza sabuni za maji ambazo alikuwa akitengeneza mwenyewe. Hakuitupa pia ndoto yake ya kucheza muziki aliyokuwa nayo hadi kupewa jina la Yondo Sister kwao Migori nchini Kenya. Katika muda wake wa jioni alianza kucheza muziki kwenye vilabu mbalimbali ambako alipata umaarufu.

Mwaka 2007, alipata bahati ya kuitwa nchini Uholanzi kwenda kutumbuiza kwenye sherehe binafsi.

“Nilipotoka huko wakanilipa $3,000,” anasema. “Kwangu ilikuwa ni fedha nyingi sana, niliporudi nilikuwa najiona tajiri sana. Hizi fedha zangu niliporudi nikazificha chini ya kitanda kwakuwa sikuwa na akaunti. Nikafikiria jambo la kufanya lakini nikarudi kwa ile ndoto yangu yangu ya utax. Nikatafuta gari second hand aina ya Nissan B14 , nikanunua na hizo laki tatu za Kenya.”

Akothee anakumbuka hadi namba ya gari yake hiyo ya kwanza kuwa ni KAT 516 F.

Anasema gari hiyo aliipenda kwakuwa ilimpatia kazi nyingi na pia ilitumika kama nyumba yake ya kulala pale alipokosa kodi ya kulipia nyumba. Awamu nyingine alienda tena nje ya nchi kufanya show kwenye private party na kurejea na takriban shilingi 250,000 za Kenya ambazo alizitumia kununua gari nyingine.

“Sasa nilikuwa na hiyo ndoto ya kumiliki kampuni ya taxi ambapo kuna magari zimepangana, mahali pesa ingetoka hiyo haikuwa shida yangu, hiyo nilimwachia Mungu,” anasema Akothee ambaye alifanya pia kazi kama dereva wa taxi kwa kipindi cha miaka mitatu.

Akothee anasema alijitokeza mtu ambaye alimpenda jinsi anavyojituma kama dereva wa taxi, anavyohudumia familia yake na uwezo wa kucheza kama dancer na kumuuliza angependa amfanyie nini.

“Nikamwambia mimi nikipata bus tu ya kama watu 23 naona huu utaxi wangu umekamilika na gari ya safari. Akawa mkarimu na nikapata huo msaada alioniambia atanipa. Pesa nilitumiwa na vilevile nilitumiwa ndio nikaenda nikanunua hivyo vitu ambavyo roho yangu ilikuwa inataka,” anakumbushia Akothee ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa kampuni ya Akothee Safaris: Tours & Travel co, Car Hire & Taxi Services.

Nyumba1
Akothee akiwa kwenye moja ya nyumba zake

Amesema mtaji wake uliendelea kuwa mkubwa na magari yaliongezeka hadi kufika zaidi ya 12. “Sasa hivi niko na bus mbili, za 27 sita, ndogo zipo kama nne, kisha sasa hivi nipo na Land Cruisers za kupeleka wageni safari, zipo tano sasa hivi.”

14947_807818472574607_8866015745327345166_n
Baadhi ya magari ya kampuni ya Akothee Safaris

Pia ameanzisha kampuni yake ya upangaji wa nyumba (real estate) akimiliki nyumba kadhaa nchini Kenya huku akiendelea kuwa na mipango mikubwa zaidi.

934839_771933776207578_1368223920584298612_n
Akothee akiwa mbele ya gari yake ya kutembelea

Pamoja na kuwa na utajiri huo unaokuwa kwa kasi, Akothee amesema muziki ni kitu anachokipenda na ataendelea kukifanya kwakuwa kinampa furaha.

“Ninafanya muziki kama passion,” anasisitiza. “Music is one of my biggest hobby and I love music, naupenda kwa ndani, nausikia kwenye mifupa.”

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents